Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa) amesema Israel inaendelea kuzuia misheni ya kibinadamu kufika kaskazini mwa Gaza ikiwa na vifaa muhimu kama chakula na dawa.
"Hospitali zimeshambuliwa na kuachwa zimelemazwa huku watu waliojeruhiwa wakiachwa bila huduma," Philippe Lazzarini aliandika kwenye mtandao wa X.
Pia alisema makazi yaliyosalia ya Unrwa yalikuwa yamejaa kupita kiasi hivi kwamba watu waliokimbia makazi "wanalazimika kuishi kwenye vyoo", na akataja ripoti kwamba watu wanaojaribu kukimbia walikuwa wakiuawa.
Jeshi la Israel limekuwa likizidisha mashambulizi ya wiki moja katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza dhidi ya kile ilichosema ni wapiganaji wa Hamas waliojikita tena huko.
Siku ya Jumatatu wakaazi na madaktari walisema vikosi vya Israel vilikuwa vinazingira hospitali na makazi ya watu waliokimbia makazi yao.