Back to top

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA KASI UJENZI UWANJA WA MPIRA ARUSHA

07 September 2024
Share

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Husna Sekiboko, imeridhishwa na maendeleo ya Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Jijini Arusha, utakaotumika kwa mashindano ya AFCON 2027.

"Sisi kama kamati tumeridhishwa sana na maendeleo ya ujenzi wa uwanja huu katika hatua ya mwanzo kabisa ambapo hadi sasa Serikali imeshatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 50, tunauona utayari wa Serikali kukamilisha mradi huu na sisi kama Bunge hatutakuwa kikwazo katika kuunga mkono jitihada nzuri ambazo zinaendelea kuwekwa na Serikali yetu"Amesema Mhe.Sekiboko

Ametoa rai kwa Serikali na mkandarasi juu ya kukamilisha mradi huo kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa huku akigusia kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Dodoma.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Damas Ndumbaro, amesema kuwa Serikali imepokea maelekezo na ushauri wa kamati na kuwahakikishia kuwa itasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi zaidi.

Ujenzi wa uwanja huo utakaotumika kwa mashindano ya AFCON 2027 tayari shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuchimba eneo la uwanja kuondoa udongo usiofaa, ujenzi wa majengo ya muda kwa ajili ya ofisi na makazi ya mkandarasi.