Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, amemtaka Mkandarasi na Mtaalamu Mshauri anayetekeleza Mkataba wa Ujenzi wa miundombinu inayoratibiwa na mradi wa TACTIC wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, kukamilisha haraka ujenzi huo kulingana na matakwa ya mkataba ili wananchi wanufaike kikamilifu na uwekezaji huo unaosimamiwa na Serikali kupitia TAMISEMI.
Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo mara baada ya kupata malalamiko kadhaa kutoka kwa viongozi mbalimbali mkoani Shinyanga, wakilalamikia mwenendo usioridhisha wa Mkandarasi M/S Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation Ltd, anayetekeleza ujenzi wa barabara za mjini, barabara ya kuingia kituo cha wajasiriamali cha Zongomela pamoja na mitaro ya kutiririsha maji ya mvua kwenye Halmashauri ya mji wa Kahama.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Katimba amemuagiza Mtaalamu mshauri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kahama kuhakikisha kuwa mikataba inasimamiwa vizuri ili kuwezesha kukamilika ndani ya muda uliopangwa, kwa ubora tarajiwa huku thamani ya fedha iliyotumika ikitakiwa kuonekana kwa ukamilifu wake.
Kufuatia maelekezo hayo, Mhe. Katimba ametembelea na kukagua miradi hiyo inayolalamikiwa na kupata maoni ya wadau mbalimbali, akiahidi Kumshauri Waziri wa Nchi- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) kuhusu hatua za kuchukua kwa Mkandarasi huyo anayesuasa katika utekelezaji wa mradi huo kwa kwenda kinyume na mkataba na hivyo kusababisha kuchelewa kwa tija ya uwekezaji huo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Katimba amemuagiza Mtaalamu mshauri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kahama kuhakikisha kuwa mikataba inasimamiwa vizuri ili kuwezesha kukamilika ndani ya muda uliopangwa, kwa ubora tarajiwa huku thamani ya fedha iliyotumika ikitakiwa kuonekana kwa ukamilifu wake.
Aidha, Mhe. Katimba alisema uboreshaji wa miundombinu ya barabara unaofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia TARURA, umepelekea ongezeko kubwa la bajeti ya TARURA kutoka Bilioni 275 hadi Bilioni 710 kwa mwaka ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 inayoelekeza kuhusu maboresho ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kuchochea shughuli za kiuchumi.
Mhe. Katimba pia amesema uboreshaji huo umewezeshwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia yenye kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo ya TACTIC suala linalosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuibua fursa mpya za ajira pamoja na kustawisha pato la wananchi na la Manispaa, Miji na Majiji ya Tanzania.
Kufuatia jitihada hizo, Mhe. Katimba amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine inapotekelezwa miradi ya TACTIC kulinda miundombinu hiyo ili kuhakikisha kuwa inatumika na jamii kwa muda mrefu.
" Wananchi tuna wajibu wa kuilinda miradi hii inayojengwa kwa gharama kubwa ili kuleta tija kwa wananchi kulingana na matarajio na malengo ya mikataba ya utekelezaji wa miradi," alisema Mhe. Katimba.