Back to top

KIJIJI CHA MNANILA BUHIGWE CHAPEWA HADHI YA MJI MDOGO

10 July 2024
Share

Kijiji cha Mnanila kilichopo tarafa ya Manyovu wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, kimepandishwa hadhi na kuwa mji mdogo ambapo sasa kijiji hicho kimewekewa mpango na kupimwa viwanja kwa lengo la kuharakisha maendeleo. 

Uamuzi huo ni hatua ya utekelezaji vipaumbele vya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi Mijini na Vijijini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda, ambaye amesema kutokana na maendeleo yanayokuwa kwa kasi kwenye mji huo mdogo wa Mnanila, wizara yake imeona ipo haja ya kuupanga ili kuharakisha kasi ya maendeleo kwa wananchi.

Mhe.Pinda amebanisha kuwa, Wizara ya Ardhi inaenda kuweka mpango ili mji huo uwe katika mpangilio mzuri wa kimji utakaovutia sambamba na kuwa na maeneo yanayokidhi mahitaji ya wananchi wa mji huo.

Amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma Palmon Martin Rwegoshora, kuhakikisha wakati wa urasimishaji makazi holela wananchi wanashirikishwa ili kuondoa migongano inayoweza kujitokeza.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mji huo mdogo wa Mnanila unaoenda kujengwa pia Kituo kikubwa na cha kisasa cha forodha ni vizuri ukaendana na miji mingine yenye vituo hivyo na wananchi wanatakiwa kuyapokea mabadiliko yanayoenda kuubadilisha mji huo

Kufuatia mpango wa uendelezaji katika mji mdogo wa Mnanila, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma Palmon Rwegoshora ameeleza kuwa, tayari michoro ya mipango miji imeandaliwa na kupatikana takriban viwanja 1000 upande wa kuelekea mpaka wa Tanzania na Burundi.