
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Kampuni ya Kili International Marathon ambao ni waandaji wa mbio za Kili marathon kuhakikisha mbio hizo zinatumika kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo mkoani Kilimanjaro wakati aliposhiriki mbio za Kili Marathon za kilomita 5.
“ Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iangalie namna bora ya kushirikiana na Kili Marathon ili mbio hizi ziwe nyenzo ya kutangaza utalii wetu na kuwa fursa kwa wageni kutembelea vivutio vyetu vya utalii,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema mbio hizo zimeendelea kuwavutia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi ambapo mwaka huu zaidi ya watu 20,000 wameshiriki mbio hizo.
Pamoja na changamoto ya ufinyu wa barabara, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali itafanya maboresho ya miundombinu ya barabara ili kutoa fursa ya washiriki kukimbia kwa nafasi.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko atoa rai kwa Watanzania kushiriki mashindano hayo kwa vile yana fursa mbalimbali ikiwemo biashara, pamoja na kuzingatia ulaji wenye afya na kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
Katika hatua nyingine, amesema mbio hizo ziwe kichocheo cha kudumisha amani na umoja miongoni Watanzania huku akiwashukuru washiriki wa mbio hizo kutoka nje ya nchi.
Vilevile, amewapongeza wadhamini wa mbio hizo ambao ni Kilimanjaro Larger, Yas na CRDB Bank.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Kili Marathon ni mbio zilizoonesha mfano na Wizara yake itaendelea kushirikiana nao ili kuzikuza zaidi.
Ameendelea kusema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau itaandaa mazjngira mazuri kwa vijana na wanamichezo wote kwa kuboresha miundombibu kwa ajili ya michezo mbalimbali nchini na kutoa fursa ya kufanya mazoezi na kushindana kimataifa.
Pia, amewapongeza washindi wote wa mbio hizo, sambamba na kulielekeza Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuandaa mpango mkakati kwa ajili ya mchezo wa riadha ili nchi iweze kupata wanariadha mahiri watakaoiwakilisha nchi kimataifa.
Aidha, washindi wa Kili Marathon wa viwango mbalimbali vya mbio walitunukiwa zawadi za fedha na medali.