Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza wakazi wa Mkoa wa Arusha wakiwemo viongozi wa dini na wadau wa Utalii kwa kuendelea kutunza amani na utulivu, suala ambalo limechangia ongezeko kubwa la idadi ya watalii pamoja na mikutano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi hizo leo Novemba 27, 2024, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Arusha, waliofika kumlaki kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA, akielekea mkoani Arusha kwenye ziara ya kikazi ya siku nne.
Amewashukuru wafanyabiashara na wadau wa utalii waliofika kumpokea na magari ya kitalii zaidi ya 500, na kusema suala hilo limekuwa la heshima kubwa kwake na linampa moyo na ari zaidi ya kuwatumikia Watanzania, akiahidi kurudi mkoani Arusha kwa ajili ya kuzungumza na wafanyabiashara na wadau hao wa utalii.
Akimkaribisha mkoani Arusha, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Christian Makonda amesema hatua ya Rais Samia kuruhusu chanjo ya Corona kuingia nchini Tanzania Julai 2021 pamoja na kushiriki kwenye Filamu ya Royal Tour mwaka 2022, kumekuwa na faida kubwa kwa uchumi na utalii wa Mkoa wa Arusha suala ambalo limechochea Pato la Mkoa wa Arusha na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Arusha kesho Alhamisi anatarajiwa kutunuku Kamisheni kwa Maafisa wanafunzi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, kushiriki kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki pamoja na kuwa na mkutano na viongozi wa jamii ya Kimasai mkoani Arusha.