Back to top

LITEMBO HOSPITALI YAPATIWA GARI NA WATUMISHI

23 April 2025
Share

Katika kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa gari moja la wagonjwa (Ambulance), wataalam wawili wa maabara, daktari mmoja pamoja na muuguzi mmoja ili kupunguza changamoto katika Hospitali ya Litembo.

Waziri Mhagama ametekeleza maagizo hayo na kumuagiza Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Danny Temba kupeleka Ambulance hiyo kabla ya kurudi Dodoma, ikiwa ni hatua za kuendelea kuboresha sekta ya afya nchini, baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Litembo pamoja na Chuo cha Sayansi Shirikishi Litembo kilichopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

"Mhe. Rais Samia baada ya kusikia changamoto hizi, alituelekeza sisi wasaidizi wake kuwaletea gari pamoja na watumishi, kwenye ajira mpya zilizotangazwa kupitia halmashauri ya wilaya ya Mbiga tutaleta daktari mmoja na muuguzi mmoja na mimi nimekuja kutekeleza maelekezo ya Rais sio kutoa ahadi,"Amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya afya kwani amejenga zahanati, Vituo vya Afya vya kisasa nchi nzima pamoja na ukarabati wa hospitali ya wilaya ya Mbinga.

Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amewataka wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Litembo, kilichopo Halmashauri ya Mbinga kuzingatia masomo yao kwa kuwa huduma wanazokwenda kuzitoa ni huduma za msingi ambazo Watanzania wanazihitaji tena zikiwa sahihi na zenye ubora.