Wachimbaji wa madini mkoani Mara wametakiwa kuachana na imani potofu za kupiga ramli na kufanya matambiko na hata wengine kudaiwa kutumia viungo vya binadamu ili waweze kupata dhahabu katika mashimo yao na badala yake wameshauriwa kujikita katika maabara za kisayansi zinazowawezesha kupata taarifa za uhakika kutoka katika mchanga uliochimbwa.
Wadau wa sekta ya madini wameamua kuleta maabara ya kisasa mkoani Mara, yenye uwezo wa kutambua sampuli zaidi ya kumi za madini kwa muda wa dakika na tano na kutoa majibu, hatua inayotajwa kuwa ni mkombozi kwa wachimbaji wadogo wadogo.
Wakielezea umuhimu wa maabara hiyo, baadhi ya wachimbaji wadogo wanakiri kwamba itakuwa msaada mkubwa kwao kwani wataepuka kuibiwa dhahabu yao.
Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk. Vicent Naano akizungumzia ujio wa maabara hiyo amepiga marufuku usafirishaji wa sampuli za madini kwenda mikoa ya Mwanza na Geita.
Ujio wa maabara za kisayansi zinazoweza kutambua sampuli za madini zilizopo katika mchanga zinatajwa kuwa mkombozi kwa wachimbaji wadogo kujiepusha na imani za kishirikina.