Back to top

Mahakama ya Kisutu yaamuru kuletwa kwa shauri la Kabendera Agosti 5

01 August 2019
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka Upande wa Serikali kuwasilisha kiapo kinzani Agosti 5, 2019 kujibu hoja kuhusu kukamatwa kwa mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera.

Maagizo hayo yametolewa na hakimu mkazi Mkuu, Augustine Rwizile baada ya Wakili kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),  Shilinde Swedy kuwasilisha maombi ya kutaka Kabendera afikishwe mahakamani kwa sababu Jeshi la Polisi linamshikilia tangu Julai 29, 2019 hadi sasa.

Katika maombi hayo namba 14 ya mwaka 2019 yaliyofunguliwa Julai 30, amedai kuwa hadi sasa saa 24 zimeshapita, hivyo anapaswa kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma zozote zinazomkabili kwa ajili ya haki zake za msingi ikiwemo  dhamana kwani kosa linadhaminika.

Katika majibu ya serikali, kupitia wakili wa serikali mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama iwape muda mpaka August 7, 2019 kwa ajili ya kuwasilisha kiapo kinzani katika maombi hayo, huku upande wa utetezi ukiomba Agosti 2, 2019.

Hata hivyo kutokana na hoja za pande zote mbili mahakama iliamuru majibu hayo yaletwe Agosti 5, 2019 saa 7 mchana.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Rwizile ameutaka upande wa Serikali  kuwasilisha kiapo kinzani Agosti 5, 2019.