Back to top

MAJAJI WATATU KUAMUA HATMA YA GACHAGUA LEO

22 October 2024
Share

Jopo la majaji watatu leo linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kuondolewa ofisini kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais.

Jopo hilo linaloongozwa na Jaji Eric Ogola pia lina majaji Anthony Mrima na Freda Mugambi na liinatarajiwa kutoa uamuzi leo ikiwa litaondoa au kuongeza muda wa maagizo ya kuzuia kuapishwa kwa Kithure Kindiki kuchukua wadhifa wa Naibu Rais baada ya uteuzi wake na Rais William Ruto na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa siku ya Ijumaa.

Hii ni baada ya majaji Chacha Mwita kutoka Milimani na Richard Mwongo kutoka Kerugoya kutoa maagizo ya kusitisha utekelezwaji wa azimio lililopitishwa na Seneti kumwondoa Gachagua ofisini kupitia kura iliyopitisha mashtaka 5 kati ya 11 dhidi yake yaliyowasilishwa kwa seneti na bunge la Kitaifa na kumzuia Kithure kuchukua usukani katika Ofisi hiyo.

Juhudi za Mwanasheria Mkuu wa serikali Dorcas Oduor kutaka maagizo hayo yaondolewe yalitupiliwa mbali na mahakama ya majaji watatu, ambayo badala yake iliamuru kusikilizwa kwa kesi baina ya pande zote Jumanne.

Wakati huo huo Idara ya DCI nchini Kenya imemtaka Gachagua kufika katika makao yake ili kutoa ufafanuzi kuhusu madai yake kwamba kulikuwa na majaribio mawili ya kumuua kutumia sumu.

Idara hiyo imesema madai hayo yana uzito na hivyo basi Gachagua anafaa kuyatolea ufafanuzi.