
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa serikali za mitaa kote nchini kujiepusha kuwa vyanzo vya migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao, akiwataka kuwa sehemu ya masuluhisho ya migogoro hiyo.
Wakati wa Mkutano mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za mitaa Tanzania Alat Ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma leo Machi 11, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo ameitaja migogoro ya ardhi kama Donda sugu kwenye jamii, akiitaja kama chanzo cha uhasana na mauaji kwenye ngazi ya jamii.
Katika hatua nyingine Rais Samia pia amewataka watendaji wa serikali za mitaa kuendelea kusimamia watumishi na watendaji wa mamlaka zao katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kuwapokea na kuwasikiliza kwa busara sambamba na kuimarisha mifumo ya ushughulikiaji wa kero za wananchi kwa wakati.
Rais Samia pia katika hotuba yake amesisitiza kuhusu kuoanisha mipango ya ngazi ya Halmashauri na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na kusisitiza juhudi zaidi katika kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato na kujiepusha na migogoro kati yao na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali na badala yake wakuze na kuimarisha mahusiano mazuri kati yao.