Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda, amezitaka taasisi zilizopewa mamlaka ya upimaji kuhakikisha zinashirikiana na Wizara ya Ardhi pale zinapokwenda uwandani ili kusaidia kuondoa migogoro inayoweza kuanzishwa kutokana na kutojua uhalisia wa mipaka.
Mhe.Pinda amebainisha hayo Jijini Arusha, ambapo ametoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe.Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa upendekeo kwa Wizara ya Ardhi hususani katika kuridhia miradi mikubwa ya maboresho ndani ya wizara.
Amesema Wizara ya Ardhi imeanza kujenga mfumo wake wa TEHAMA wenye lengo la kufanya maboresho yatakayowezesha kuwa na ardhi kiganjani ili kuondoa changamoto za sasa kama vile uwepo viwanja pandikizi sambamba na kuwezesha wananchi kupokea taarifa pamoja na kuwasilisha malalamiko na maombi ya viwanja kupitia ardhi mtandao jambo alilolieleza litaondoa vishoka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mansoor Hamdoun amesema, wizara ya Ardhi inaendeea na mikakati ya kuhakikisha inaboresha huduma zinazotolewa na wizara ikiwemo sehemu ya idara ya upimaji na ramani aliyoieleza kuwa ni idara kongwe katika wizara hiyo.
Ametanabahisha kuwa, ipo miradi mikubwa miwili ukiwepo wa ule wa milki salama za ardhi unaotokana na mkopo wa Benki ya Dunia aliouleza kuwa unatarajia kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi ikiwemo eneo la upimaji na ramani.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasi ya Wapima Tanzania (IST) unashirikisha wataalamu wa upimaji na ramani kutoka wizara ya ardhi, taasisi za umma pamoja na kampuni binafsi ambapo mbali na mambo mengine mkutano huo utatumika kufanya uchaguzi wa viongozi wa Taasisi hiyo.