Back to top

"Marufuku fomu za maadili za viongozi wa Umma kujazwa Mtandaoni" -JPM

24 December 2020
Share

CHAMWINO, DODOMA.

Rais Dkt.John Pombe Magufuli amemuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe.Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili, hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.

Akizungumza baada ya kumuapisha, Rais Magufuli amemtaka akaendeleze kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Marehemu Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Harold Nsekela.

Rais Magufuli amewasisitiza viongozi wote wa umma takribani elfu kumi na tano wanaotakiwa kujaza fomu za maadili, wafanye hivyo kabla ya tarehe 30 Disemba 2020 kwa mujibu wa sheria na kwamba ndiyo maana amemteua, Kamishna wa Maadili, Mhe.Mwangesi kujaza nafasi iliyoachwa na marehemu Nsekela ili kusiwe na visingizio.

Aidha ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya viongozi iachane na ujazaji na uwasilishaji wa fomu za maadili ya uongozi kwa njia ya mtandao, ili kuepusha uvujaji wa siri na ubadilishaji wa maudhui ya fomu hizo na badala yake fomu zichukuliwe mtandaoni na kisha kujazwa na kuwasilishwa nakala halisi kwa ofisi husika.

Rais Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya Krismasi na Mwaka Mpya na kuwataka viongozi na watumishi ambao hawana zuio la Waziri Mkuu waruhusiwe kwenda makwao kusalimu ndugu na jamaa wakati huu wa sikukuu.