Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti, amesema Serikali itaendelea kutounga mkono wafugaji wanaofuga kimila badala ya ufugaji wa kisasa unaoweza kuboresha uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Mnyeti amesema hayo wakati akifungua maonesho ya Mnada wa Mifugo yaliyofanyika kwenye Viwanja vya 'Mbogo Ranch' eneo la Ubena Zomozi Mkoani Pwani ambapo amebainisha kuwa mbali na ufugaji huo kupitwa na wakati, mifugo yake haina sifa ya kuuzwa kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema "Ni lazima tuambiane ukweli, Mimi sipendi kumung’unya maneno kwa sababu Mhe. Rais amenipa kazi ili niwaambie ukweli kwamba ng’ombe wote mnaowafuga msipowachanja na kuwaogesha hawana sifa ya kuliwa na binadamu awe Tanzania au nje ya hapa"
Aidha Mhe. Mnyeti amewataka wafugaji wote waliofika kwenye Maonesho hayo kujifunza kwa makini elimu ya vitendo inayotolewa kuhusu ufugaji wa kibiashara viwanjani hapo ili wakabadili mfumo wa ufugaji kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ambao ndio wadhamini wakuu wa Maonesho hayo Bw.Frank Nyabundege amebainisha kuwa kwa kuzingatia tija wanayopata wafugaji kupitia maonesho hayo benki yake itaendelea kuyadhamini ili kubadili hali ya ufugaji nchini na kuwafanya wafuge kibiashara.
"Mpaka sasa benki yetu imeshatoa takribani Bil.25 kwenye sekta ya Mifugo ambayo tumeielekeza kwenye mnyororo wa thamani wa Unenepeshaji na ng’ombe wa maziwa hivyo vijana wote mnaotaka kufuga njooni kwetu kwa sababu kupitia riba ndogo sana tunawawekea mifumo mizuri ambayo mtaenda kufaidika nayo wakati wote" Amesema Bw. Nyabundege
Akielezea lengo la kuandaa Maonesho ya Mnada wa Mifugo nchini, Mratibu wa Maonesho hayo Bw. Naweed Mulla amesema kuwa maonesho hayo yanalenga kuwanyanyua wananchi na kuwathibitishia kwa vitendo kuwa ufugaji bora kibiashara unawezekana hapa nchini.
Maonesho ya Mnada wa Mifugo mwaka huu yaliyobebwa na kauli mbiu ya “Fuga Kibiashara, Tujenge Kesho iliyo Bora” yanatarajiwa kufikia tamati Juni 16, 2024 ambapo Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Doto Biteko anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ya ufungaji.