Back to top

MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI WAFIKIA ASILIMIA 47

22 November 2024
Share

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,  Dkt. James Mataragio amesema nchi za Tanzania na Uganda zitaendelea kushirikiana katika uendelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati ikiwemo Sekta ya Mafuta na Gesi.

Dkt. Mataragio ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa habari  baada ya kushiriki Jukwaa la Kibiashara kati ya Tanzania na Uganda .

"Tunaangalia ni kwa jinsi gani sekta hii ya Mafuta na Gesi inaweza ikachangia katika maendeleo ya Nchi hizi mbili, tumekuwa na mijadala mbalimbali inayolenga kuiendeleza sekta hii ya mafuta na gesi." Amesema Dkt. Mataragio 

Ameongeza kuwa, mjadala  mkubwa katika Jukwaa hilo ni kuangalia namna gani Nchi za Tanzania na Uganda zinaweza kushirikiana katika sekta za mafuta na gesi. Huku akibainisha mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi (EACOP), umefikia asilimia 47.

Mataragio amesema Tanzania na Uganda zinahistoria ndefu ndefu za mashirikiano akitolea mfano mradi wa kimkakati wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi wa EACOP.

Amesisitiza kuwa mradi huo kwa sasa upo katika hatua ya kutandaza mabomba ambapo takribani kilomita 52 za mabomba zimesha chomelewa ambazo zitaanza kufukiwa ardhini.

Akizungumzia faida ya mradi kwa wananchi amesema watanzania wameweza kujengewa uwezo (Capacity building) katika maeneo mbalimbali na hivi sasa wanafanya kazi kwenye mradi huo.

Kwa upande wa ajira amesema mradi umeweza kutoa zaidi ya ajira 8000 huku lengo likiwa ajira 10,000.