Back to top

MSAADA WA KISHERIA SULUHU YA MIGOGORO ZANZIBAR

23 April 2025
Share

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman, amewasihi wananchi wa Kaskazini Unguja Visiwani Zanzibar, kujitokeza kwa wingi kupata msaada wa Kisheria kwenye Mkoa huo itakayodumu kwa siku tisa, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia kwa ubunifu na ufadhili wa kampeni hiyo, aliyoitaja kuwa muhimu kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kiuchumi.

Mhe. Haroun ambaye amekuwa Mgeni rasmi katika uzinduzi huo leo kwenye Uwanja wa Tumaini Skuli ya Mkwajuni Kaskazini Unguja, akieleza matarajio yake kuwa Kampeni hiyo itaondoa misururu mirefu ya wananchi wanaofuata majawabu ya Changamoto zao mbalimbali za kisheria kwenye Ofisi za wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kwa upande huo wa Zanzibar.

"Wanyonge walikuwa hawana uwezo na tunawajua, wanapata shida sana wanapodai haki zao, sasa muarobaini umepatikana. Kuna matatizo mengi mnayo, matatizo ya ardhi, lakini hata wafanyakazi mnaofanya kazi katika mahoteli na maeneo mengine mnahitaji msaada wa kisheria kwani pengine kuna haki zao nyingi wanazikosa, wanafanyishwa kazi kinyume na taratibu, sasa hii ni fursa muhimu kuhakikisha mambo hayo tunayapunguza ama tunayamaliza kabisa." Amesema Mhe. Waziri.

Amesisitiza kuwa matatizo mengi na migogoro ya kijamii inasababishwa na Uvunjifu wa sheria unaofanywa na baadhi ya watu, Mhe. Haroun, amemshukuru pia Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania bara, Mhe. Damas Ndumbaro kwa namna Wizara yake imekuwa ikishirikiana na Wizara yake katika masuala mbalimbali, akiomba Ushirikiano huo uendelee na ufanyike kwenye Wizara nyingine, kama sehemu ya kusaidia ustawi wa wananchi wa pande mbili hizi za muungano suala ambalo litaimarisha pia muungano.

Katika hatua nyingine, Mhe. Haroun amewahimiza wananchi wa Zanzibar na Tanzania bara kuendelea kuilinda na kuitunza amani ya Tanzania kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu, akieleza kuwa upatikanaji wa haki umeegemea zaidi katika amani na utulivu kwani kukosekana kwake, Haki hukandamizwa na sauti za wananchi kutosikika kwenye vurugu.