Back to top

MTHAMINI MKUU WA SERIKALI ATAKA UADILIFU KATIKA UTHAMINI

11 December 2024
Share

Mthamini Mkuu wa Serikali Bi. Evalyne Mugasha amewataka Wathamini nchini kuwa makini na kazi zao na kufanya kazi kwa uadilifu ili kuepuka migogoro inayotokana na kazi zao.

Bi.Evelyne amesema hayo leo tarehe 11 wakati akizungumza na Wathamini pamoja na Warasimu Ramani wa Wizara ya Ardhi wanaopata mafunzo kwa ajili ya zoezi la uandaaji vitalu vya thamani ya ardhi ( Valuation  Block) yaliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

"Hakuna uthamini mbaya cha msingi ni kuwa makini na kazi zenu na kuhakikisha mnafanya kazi kwa umakini na uadilifu huku mkizingatia sheria na miongozo ya taaluma zenu ili kuepuka malalamiko dhidi yenu" amesema Bi Evelyne.

Amesema, mafunzo wanayoyapata watumishi hao wanatakiwa kuyachukulia kwa umakini mkubwa kwa kuwa yanawapeleka kwenye mfumo wa kidigitali (e-ardhi) alioueleza kuwa, kwa kiasi kikubwa unaenda kuondoa dhana ya udanganyifu unaoweza kutokea wakati wa kazi zao.

Kwa mujibu wa Mthamini huyo Mkuu wa Serikali, watumishi wanaochukua mafunzo hayo wanatakiwa kubadilika kiutendaji huku akiwaasa kutokubali kubadilishwa na badala yake wabadilike wenyewe huku wakifanya kazi kwa kuzingatia maadili kwa kuwa uthamini unagusa watu wengi.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo Bw. Baraka Mollel amesema, mafunzo  yanyotolewa ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo Wathamini na Warasimu Ramani wa wizara ya ardhi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hasa  kipindi hiki ambacho Wizara ya Ardhi imeboresha mifumo yake na kuwa ya kidigitaki.

Kwa mujibu wa Bw. Mollel, vitalu vya thamani ya ardhi vitajumuishwa kwenye mfumo wa e- ardhi utakaowezesha ulipaji tozo mbalimbali ikiwemo kodi ya ardhi, kodi ya ongezeko la thamani na tozo nyingine zinazotokana na thamani.

"Mafunzo ya uandaaji vitalu vya thamani kwa Wathamini na Warasimu Ramani yatawezesha kujumuishwa kwa vitalu kwenye mfumo wa e-ardhi na kuwezesha ulipaji tozo mbalimbali ikiwemo kodi ya ardhi na tozo nyingine zitokanazo na thamani" amesema Bw. Mollel.

Aidha, Bw. Mollel ameongeza kuwa, mafunzo hayo yatasaidia katika utekelezaji wa shughuli za uthamini kama vile rehani, uhamishaji milki na uthamani kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya serikali.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza matumizi ya mifumo ya kidigitali (e-ardhi) ambapo hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi

Waziri wake Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanatumia mfumo huo katika maeneo ambayo mfumo huo umeanza kutumika.

Mfumo wa e-Ardhi umeanza kutumika kwenye wmaeneo mbalimbali nchini kama vile Dodoma, Arusha, Tabora katika halmashauri ya Nzega, Pwani halmashauri ya Chalinze pamoja na manispaa ya Shinyanga na Kahama zilizopo mkoa wa Shinyanga.