Back to top

MTWARA KUNUFAIKA NA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA

23 July 2024
Share

Wananchi wanaohitaji mikopo mkoani Mtwara, wameshauriwa kwenda kukopa kwenye taasisi rasmi zilizosajiliwa kisheria, kwa ajili ya usalama wa fedha zao.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, wakati akizungumza na wataalamu wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na taasisi shiriki, waliomtembelea ofisini kwake.

Ameipongeza Wizara ya Fedha kufuatia mpango wake unaolenga kuwapa wananchi uelewa wa masuala ya Fedha ikiwemo Usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji akiba uwekezaji, kinga za kibima na Mikopo iliyo salama kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.

Aidha, amewaasa watoa Huduma Ndogo za Fedha Mkoani Mtwara na kwingineko kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019, na kuonya kuwa watakaotoa huduma hizo bila kufuata sheria watawajibishwa kwa mujibu wa sheria tajwa. 

Kwa upande wake Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi, kutokana na wengi wao kuwa na matumizi yasiyo sahihi pale wanapopata fedha.

"Programu hii inalenga kuwafikia wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali, ili pamoja na mambo mengine wafahamu maeneo rasmi ya kupata huduma za fedha namna ya kuzisimamia fedha zao pamoja na kujiwekea utaratibu wa kuweka akiba na kuwekeza  kwa ajili ya kupata faida endelevu.  amesema Kimaro.