Back to top

NAIBU WAZIRI KAPINGA ATAKA KASI YA UUNGANISHAJI UMEME USHETU IONGEZEKE

02 July 2024
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi ya kuwaunganishia umeme wananchi  katika vijiji ambavyo tayari vimefikiwa na miradi ya usambazaji umeme ili kuleta tija.

Kapinga ameyasema hayo  tarehe 1 Julai, 2024 wakati alipokagua miradi ya umeme katika  Vijiji Vya Nimbo, Sunga na Nyawishi vilivyopo Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.

“Haipendezi kuona mradi umefika katika kijiji na umekamilika lakini unakuta kaya tano au kumi  zimeunganishwa, hii hailingani na nguvu iliyotumika kuufikisha mradi  katika Kijiji, hivyo angalieni upya namna bora ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hii." Amesisitiza Kapinga

Aidha, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga Kuhakikisha wanaunganisha umeme kwenye taasisi  ikiwemo Hospitali, Shule na miradi ya maji  ili kuwezesha wananchi  kupata huduma bora za kijamii.

Pia, Mhe. Kapinga amewahakikishia wananchi wa kijiji cha Sunga kuwa watapata umeme ndani ya siku Tisa kuanzia sasa.

“ Wananchi wa Kijiji cha Sunga ifikapo tarehe 10 mwezi Huu mtakuwa mmepata umeme kwa sababu Mkandarasi ameshalipwa kila kitu na niahidi kuwa tutafikisha umeme kila sehemu ndani ya nchi kuanzia wilayani hadi vitongojini kwa sababu Rais Dkt. Samia ana nia ya dhati  kuwapa huduma ya nishati watanzania wote." Amesema Kapinga

Vilevile Kapinga ametoa wito  kwa wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

" Nawaomba tutunze miundombinu hii ya  umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu pamoja kutuletea tija katika shughuli zetu za maendeleo." Amesema Kapinga

Kwa upande wake,  Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius  Mtatiro ameshukuru kwa kazi ya usambazaji umeme katika maeneo mbalinbali nchini na  kumpongeza Mbunge wa Jimbo la ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani kwa kuwajali Wananchi kwa kuhakikisha anawapatia Maendeleo kwa Wakati.