Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda anashiriki Kongamano la Kimataifa kuhusu Miji linalofanyika Vienna nchini Austria.
Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu ya "Suluhu Bunifu kwa Miji ya Kesho” linafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Vienna, Austria kuanzia tarehe 9 hadi 11 Oktoba 2024 na kuhusisha viongozi na wataalamu wanaohusika na masuala ya usimamizi wa ukuaji na uendelezaji miji kutoka nchi mbalimbali.
Kupitia kongamano hilo, mhe. Pinda aliwaeleza washiriki namna serikali ya Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inavyofanya jitihada kukuza na kuendeleza miji.
Amezitaja baadhi ya jitihada hizo kuwa, ni pamoja na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma, Matumizi ya Mifumo ya Kielektroniki kwenye masuala ya ardhi, Uanzishwaji Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo cha Taarifa za Kijiografia pamoja na maboresho mbalimbali ikiwemo ya Sera ya Taifa.
Amelishukuru Shirika la Kimatifa la Maendeleo ya viwanda (UNIDO) kuandaa kongamanao hilo muhimu lililowakutanisha pamoja viongozi wanaohusika na masuala ya usimamizi wa ukuaji na uendelezaji miji kushirikishana ubunifu na mbinu mpya ya uendelezaji wa miji ya kesho
Lengo la mkutano huo ni kujadili na kushirikishana juu ya Suluhu bunifu kwa miji ya kesho pamoja na kutoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu kwa mustakabali endelevu wa miji kwa watu wote duniani.