Back to top

NDEJEMBI AAGIZA WATUMISHI 7 ARDHI KUCHUKULIWA HATUA

26 October 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi,  amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi saba wa wizara hiyo Mkoa wa Dar es Salaam kwa tuhuma za makosa waliyofanya kwenye sekta ya Ardhi.

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam,  wakati alipokutana na watumishi hao ambao wamekiri kuhusika na baadhi ya migogoro ya ardhi katika Mkoa huo ambapo kupitia kikao hicho  Waziri wa Ardhi amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuihusisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kushughulikia suala hilo.

Baadhi ya changamoto katika sekta ya ardhi mkoa wa Dar es Salaam, zimebainika baada ya watumishi wanaotuhumiwa  kukiri kuhusika moja kwa moja na tuhuma zinazowakabili kufuatia kupitiwa kwa majalada ambayo watumishi hao walikua waliyafanyia kazi. 

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera pamoja na watendaji wengine wa wizara.