Back to top

NDEJEMBI AMRUHUSU DAMIANO KUENDELEZA ENEO LAKE

06 October 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi ameelekeza mkazi wa Karatu mkoani Arusha mwenye viwanja Block 'J', Bw. Desderi Damiano kuendeleza eneo hilo kwa shughuli za maendeleo kufuatia Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kushindwa kumlipa fidia baada ya kutwaa eneo lake.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo wakati alipotembelea na kujionea eneo la viwanja hivyo  mara baada ya kuwasikiliza wananchi wa Karatu Mjini mkoani Arusha kwenye Kliniki ya Ardhi iliyofanyika mjini humo, ambapo amebaini Bw. Damiano kunyimwa haki ya kiwanja chake na hivyo kushindwa kukitumia kwa muda mrefu.

"Huyu ndiyo mmiliki wa asili wa eneo hili, hajawahi kulipwa fidia kwa nini mnamzuia kuendeleza eneo ambalo ni mali yake?  Eneo hili ni la kwake mpaka Halmashauri mtakapomlipa fidia mzee huyu, hivyo naelekeza aendelee na kazi zake kama alivyokua amepanga" Amesema Waziri Ndejembi.

Mmliki wa eneo hilo alizuiliwa kuliendeleza viwanja vyake  licha ya Halmashauri hiyo ya Karatu kutomlipa fidia katika eneo lake  lililopangwa kwa ajili ya matumizi ya eneo la wazi.

Aidha, Waziri Ndejembi ameelekeza Afisa Ardhi Joseph Madangi Jumatatu Oktoba 2024 aripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu na kueleza alipataje Hati ya Miliki katika eneo linalodaiwa ni la wazi na kuendelea na ujenzi huku wakimnyima Bw. Damiano umiliki wa eneo hilo.

Awali Waziri Ndejembi ametoa hati miliki za ardhi kwa wanachi waliofika katika Kliniki ya Ardhi iliyofanyika viwanja vya Mazingira Bora vilivyopo kwenye mji wa Karatu mkoani Arusha.