Back to top

NDUMBARO AFUNGUA MKUTANO WA MAWAZIRI WA SHERIA AFRIKA

22 December 2024
Share

Waziri  wa Katiba na Sheria Mhe.Dkt. Dismas Ndumbaro, amefungua  kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Sheria Barani Afrika kwa lengo la kupitia Itifaki 12 ambazo zimewasilishwa kutoka Kamati mbalimbali za kisekta kwa ajili ya kujadiliwa na kupitia mapendekezo ya Wataalamu.

Kikao hicho kilichotanguliwa na kikao cha Wataalamu kuanzia tarehe 14 Desemba,  2024  kikifuatiwa na kikao cha Mawaziri kuanzia tarehe 21-22 Desemba, 2024 katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar  nyaraka 12 zitapitiwa ambapo katika nyaraka hizo zipo baadhi ya nyaraka ambazo timu ya Wataalamu wamekubaliana lakini zipo baadhi ambazo zimepelekwa katika ngazi ya Mawaziri ili zijadiliwe, kuzipatia ufumbuzi na hatimaye kupelekwa mbele katika vyombo vya maamuzi. 

"Niwapongeze kamati ya Wataalamu kwa kazi ngumu ambayo imefanyika kwa muda wa siku saba kupitia nyaraka zote na kuziwakilisha kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Sheria na wenye dhamana ya Haki barani Afrika ili kuzipitia na kupeleka mbele katika vyombo vya maamuzi. Kati ya nyaraka hizo zipo nyaraka tisa zinazohusu zinazohusu itifaki ya biashara kidigitali barani Afrika, masuala ya Haki za Binadamu na masuala ya majanga."Alisema Waziri Ndumbaro 

Waziri Ndumbaro amesema  kuwa kupitia Itifaki 9 zinazohusu biashara ya kidigitali duniani na barani Afrika inaonesha dhahiri ni kwa namna gani Wanachama wa Umoja wa Afrika wanapaswa  kukumbatia fursa hiyo ya Mchumi wa kidijitali  ambao hauheshimu mipaka ya kijiografia na unaoifanya dunia kuwa Kijiji na kusema kuwa ni muda sasa kuweza kuzitumia kwa manufaa ya uchumi wa bara la Afrika. 

Miongoni mwa mambo makubwa yanayotarajiwa kufikiwa katika kikao hicho ni pamoja na kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Kamati ya Mawaziri wa Sheria Barani Afrika ambapo kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataraji kuchukua kiti cha uongozi wa Mawaziri wa Sheria ambapo jumla ya Nchi 38 zimeshiriki katika kikao hicho.