Back to top

NMB, ZASCO KUWAINUA WAKULIMA WA MWANI.

05 August 2024
Share

Asasi ya NMB Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) wamezindua mafunzo endelevu kwa Wakulima wa Mwani Unguja na Pemba, ambapo Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar (SMZ) imeipongeza na kuitaja asasi hiyo kama mbia wa karibu, wa kimkakati na wa muda wote wa maendeleo Zanzibar.
 
Mafunzo hayo ya miezi mitatu kwa wakulima zaidi ya 1,300 kutoka vikundi 72 vya wakulima, yamefunguliwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, yakiwa ni zao la makubaliano ya ushirikiano yaliosainiwa Machi mwaka huu kati ya NMB na Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO).
 
Akifungua mafunzo hayo, Waziri Omar alizipongeza NMB Foundation na ZASCO kwa kuyaingiza makubaliano yao katika vitendo kwa lengo la kuelimisha wakulima juu ya kilimo cha kisasa, upatikanaji mikopo nafuu ya kilimo na kuwajengea uwezo wa elimu ya fedha kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ZASCO, Masoud Rashid Mohammed, alisema mafunzo hayo sio tu zao la makubaliano ya taasisi zao katika kukuza uzalishaji wa mwani, bali ni uthibitisho wa mlinganyo wa kimalengo waliyonayo, huku akizitaka taasisi zingine za fedha kuiga mfano wa NMB.

Naye Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna, alimshukuru Waziri Omar Shaaban kwa kuwa sehemu ya hafla ya awali ya kusainiwa makubaliano na hatimaye ufunguzi wa mafunzo hayo, akisema ushiriki huo unaakisi dhamira ya SMZ katika kuwaletea maendeleo ya Wazanzibar.