Back to top

North Mara yapigwa faini ya bilioni 5.6 kwa uchafuzi wa mazingira

17 May 2019
Share

Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC), limeupiga faini ya shilingi bilioni 5.6 mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara kwa kushindwa kudhibiti utiririshaji wa maji yenye kemikali kutoka katika bwawa la kuhifadhia tope sumu na kwenda kwenye mazingira na makazi ya watu na hivyo kuhatarisha afya za wakazi wanaozunguka mgodi huo.

Kabla ya NEMC kutoa uamuzi huo, wakazi wa Nyamongo wamewalaki kwa malalamko waziri wa madini Dotto Biteko na waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais muungano na mazingira January Makamba waliotembelea mgodi huo, wakiwa wameambatana na timu ya wataalam wa serikali.

Mkurugrenzi mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Mafwenga, amesema pamoja na faini hiyo, mgodi pia unatakiwa kurekebisha kasoro zilizobainika na kujenga bwawa mbadala kudhibiti maji taka hayo yenye kemikali zenye sumu.

Wakizungumza kwa kupokezana, waziri wa madini Dotto Biteko amesema siyo nia ya serikali kuwaadhibu, kuwapiga faini au kufungia shughuli za wawekezaji lakini imebidi kuchukua hatua hizo ili kulinda maisha ya wananchi, mazingira, sheria na usalama, huku waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais, muungano na mazingira January Makamba akieleza sababu za faini hiyo kuwa kubwa kiasi hicho.

Septemba 7 mwaka jana, rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli alifanya ziara katika kijiji cha Nyamongo wilayani Tarime ambapo aliliagiza baraza la usimamizi wa mazingira kufanya utafiti wa kina juu ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na shughuli za mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara kwa takribani miaka kumi iliyopita.