Mshtakiwa namba moja katika kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino Asimwe Novert, Padri Elpidius Rwegoshora, jana alianza kujitetea na kudai kuwa ana matatizo ya kusahau.
Hatua hiyo ilisababisha Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Emmanuel Ngogwana, anayesikiliza kesi hiyo, kusitisha mwenendo wa kesi hiyo kwa siku 42 ili apelekwe katika Taasisi ya Akili Isanga kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya ya akili.
Jaji Ngogwana alitoa uamuzi huo jana wakati kesi namba 25513/2024 inayowakabili washtakiwa tisa, akiwamo padri huyo ilipofikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
Awali, akimwakilisha mshtakiwa huyo pamoja na wenzake wanane mahakamani hapo, Wakili Projestus Mlokozi aliyeteuliwa na Serikali kuwa mtetezi wa washtakiwa hao, aliomba kusitishwa kwa muda uendeshaji wa kesi hiyo ili mahakama itoe kibali kwa mujibu wa sheria, dhidi ya mtuhumiwa huyo kwenda hospitalini kuangaliwa afya ya akili, kwa kuwa wakati akifanya  mazungumzo alionekana kuwa ana tatizo.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mawakili wenzake wawili upande wa utetezi, kisha Jaji Ngingwana alipoanza kumhoji kwa maswali ya uelewa, aliridhia mtuhumiwa huyo kuchunguzwa akili.
Mahojiano kati ya Jaji Ngogwana na Padri Rwegoshora yalikuwa kama ifuatavyo;-
Jaji: Kwa nini upo mahakamani?
Padri: Niliambiwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kagera kuwa niliua mtoto.
Jaji: Tangu umezaliwa uliwahi kuwa na tatizo la afya upande wa akili?
Padri: Nina tatizo la kusahau na nilisimamishwa kazi kutokana na tatizo hilo.
Baada ya mahojiano hayo, Jaji Ngongwana alisema mahakama haiwezi kuendelea na washtakiwa wengine wanane wanaohusika na kesi hiyo mpaka Padri Rwegoshora atakapofanyiwa uchunguzi.
Jaji aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 11, mwaka huu, itakapotajwa baada ya uchunguzi wa hospitali kukamilika.
Mei 30, mwaka huu, Asimwe alichukuliwa nyumbani kwao, Kata ya Kamachumu, Muleba, mkoani Kagera na Juni 17, mwaka huu, alikutwa kwenye karavati akiwa ameuawa huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.