Back to top

PROF SEDOYEKA AKANA KUTUMIA VIBAYA OFISI

16 October 2024
Share

Baraza la Maadili limeanza kusikiliza  malalamiko dhidi ya tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (TAA), Prof. Emilian Sedoyeka, anayetuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi hiyo, kinyume na kanuni na taratibu za maadili ya uongozi wa umma.

Akiwasilisha taarifa yake katika Baraza la Maadili dhidi ya tuhuma zinazomkabili Prof Sedoyeka , Wakili wa serikali  Emma Gellan, amesema kiongozi huyo anatuhumiwa kwa  kushindwa  kutimiza matakwa ya sheria ya maadili ya umma kifungu cha 6(1)c  na kifungu cha 12(1).vya sheria  maadili ya uongozi wa umma.

Wakili Mkuu wa serikali Emma Gellan, amesema mlalamikiwa anatuhumiwa na mashtaka manne ikiwamo kumpandisha cheo  Bw. Hakimu Ndatama, kutoka Afisa Rasilimali  kuwa Mkuu wa sehemu ya rasilimali watu,  kabla ya kukamilika kwa  uhamisho wa mtumishi huyo  na bila kuwa na sifa.

Hata hivyo wakili wa serikali amesema mlalamikiwa ana uhusiano wa karibu na Bw. Hakimu Ndatama  kwa kufanya naye kazi  Chuo cha Uhasibu Arusha,  na Wizara ya Maliasili na Utalii,  na aliporudishwa tena Bw. Hakimu Ndatama  aliombewa ahamie Chuo cha Uhasibu Arusha na  mara tu baada ya  mlalamikiwa kuteuliwa  kuongoza chuo hicho, ambapo amesema matendo hayo ni kinyume na  kifungu  cha sita moja.

Tuhuma nyingine  anayokabiliwa nayo Prof.Sedoyeka ni kuingilia  mchakato wa zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza,  katika kampasi ya Babati kwa kuifuta  bila kufuata utaratibu  na bila sababu za kisheria ziliainishwa, chini ya kifungu cha 59 2 cha sheria ya ununuzi wa umma sura ya 410.

Tuhuma nyingine ni kwamba mlalamikiwa  wakati akitekeleza majukumu yake  ya uongozi wa umma, alifanya uhamisho  wa ndani wa mtumishi Bw. Robert Mwitango  Afisa Ugavi kutoka kitengo cha ununuzi na ugavi, kwenda  idara ya maktaba tofauti na sifa za kitaaluma  za mtumishi huyo.

Baada ya kusomewa tuhuma zinazomkabili mlalamikiwa Prof Emilian Sedoyeka amekana tuhuma hizo zote nne  zilizowasilishwa mbele ya baraza.