Back to top

PROF. SEDOYEKA ATUMIA SAA 3 KUPANGUA TUHUMA ZINAZOMKABILI

18 October 2024
Share

Mkuu wa Chuo katika Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka ametumia zaidi ya saa tatu kutoa utetezi wake kwa Baraza la Maadili katika tuhuma nne zinazomkabili na kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake siku zote, ametanguliza maslahi ya chuo na taifa.

Utetezi huo ameutoa kwenye kikao cha baraza hilo jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Baraza Jaji Mstaafu Rose Temba na upande wa mlalamikaji uliwakilishwa na mawakili wa serikali Emma Gellan na Hassan Mayunga.

Prof. Sedoyeka anadaiwa kukiuka maadili ya viongozi ya umma kwa kumpandisha cheo mtumishi kwa upendeleo,  kuingilia mchakato wa ununuzi wa viti na meza kampasi ya Babati, uhusiano wa karibu na mtumishi na kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi.

Akitoa utetezi wake, Prof. Sedoyeka amesema hakuwa na mamlaka ya kumpandisha cheo cha kitaaluma mtumishi hakimu Ndatama na alichofanya ni uteuzi wa kumpatia majukumu ya kuwa mkuu wa sehemu na sio Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji.

Kuhusu kuwa na uhusiano wa karibu na mtumishi huyo, Prof. Sedoyeka alisema hajahusika kwa namna yoyote kumrejesha hakimu kwenye chuo hicho kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo awali alihamia na kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu wakati akitumikia nafasi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Akizungumzia tuhuma ya kuingilia mchakato wa zabuni, Prof. Sedoyeka amefafanua kuwa dhana iliyokuwa imejengeka chuoni hapo ni kutumia mzabuni mmoja lakini akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, alijifunza kuwa zabuni inafanywa kwa ushindani na kuna kampuni nyingi zinazoweza kutoa huduma bora zaidi na kwa bei nafuu.

Amesema katika zabuni hiyo kuna wazabuni ambao walitoa bei nafuu kuliko ambaye alikuwa amepitisha ambaye ni kampuni ya Jaffer na bei yake kwa kiti na meza ni sh. 440,000 huku Timber ilikuwa sh.389,000 na Vadeck ni sh.346,000.

kuhusu kumhamisha mtumishi wa idara ya ugavi, Robert Mwintango (Afisa Ugavi) kumpeleka maktaba, amesema alifanya kwa nia njema na ni uhamisho wa kawaida wenye kuongeza ufanisi kwenye kitengo husika.

Akihitimisha kikao hicho, mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Teemba amesema wamepokea ushahidi wa pande zote mbili na baraza limekamilisha kazi yake na baada ya uchambuzi litawasilisha taarifa yake sehemu husika.