Back to top

PSSSF YATOA TZS MILIONI 10, CRDB MARATHON 2024.

16 August 2024
Share

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa msaada wa shilingi milioni 10 kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini, kupitia mbio za CRDB Marathon.

Akikabidhi msaada huo Makao Makuu ndogo ya PSSSF jijini Dar Es Salaam, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Bw. Yesaya Mwakifulefule amesema, PSSSF imeungana na CRDB ili kusaidia juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya na hivyo kusambaza tabasamu kwa wenye uhitaji na jamii nchini, ambapo fedha zitakazopatikana zitakwenda kuwasaidia watoto wenye maradhi ya moyo na akina mama wanaougua Fistula.

“Sisi tunaamini, miongoni mwa watoto watakaotibiwa, miongoni mwa akina mama watakaotibiwa wako wanachama wetu ambao kupitia mbio hizi tunakwenda kuwagusa sisi peke yetu tungehitaji fedha nyingi kufanikisha suala hili, lakini tunapoungana pamoja, sisi PSSSF, CRDB na wadau wengine wanaounga mkono mbio hizi basi changamoto za watoto na akina mama hawa zinakwenda kutatuliwa.” Bw. Mwakifulefule.

Akitoa neno la shukrani, mwakilishi kutoka CRDB Bank Bi. Joycelean Makule, ameishukuru PSSSF kwa msaada huo ambao amesema unakwenda kusaidia mipango muhimu ya afya ili kusaidia jamii ya Watanzania.
“Mbio hizi zimeanzishwa ili kuhakikisha watanzania wenyewe tunajenga utamaduni wa kuweza kutatua matatizo yanayotuzunguka, na hili tumeona ni jukwaa zuri kushirikiana na watanzania, na mwaka huu tumeweza kushirikiana na jumla ya watu 8000.”

Aidha, amesema mbio za CRDB Marathon zinatarajiwa kufanyika Agosti 18, 2024, jijini Dar Es Salaam.