Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendelea kutoa huduma kwa wananchama na wanachama kwa ujumla wakati huu wa Maonesho ya Nanenane 2024 yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Pia PSSSF wanatoa huduma kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar kwenye viwanja vya Dole, Unguja.
Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano, PSSSF, Bi. Rehema Mkamba amesema Maonesho hayo ni fursa nzuri kwa Mfuko kukutana na Wanachama wake, wakiwemo wananchi ili kutoa huduma ikiwa ni pamoja na elimu ya hifadhi ya Jamii.
Alisema Mwanachama akifika kwenye mabanda ya PSSSF, ataweza kupata taarifa za Michango, Taarifa za Mafao, Taarifa za Uwekezaji unaofanywa na Mfuko na Wastaafu wataweza kujihakiki.
“ Kama mjuavyo Mfuko umetehamisha shughuli zake, hivyo sambamba na kutoa huduma pia tunaendelea kutoa elimu ya matumizi ya teknolojia katika kupata huduma zote hizo nilizotaja. Tumeanzisha PSSSF Kidijitali, kupitia simu janja, Mwanachama anaweza kuwasilisha Madai mbalimbali, lakini pia wastaafu nao wanaweza kujihakiki.” Alifafanua.
Aidha, Amewahakikishia wanachama wakiwemo wastaafu kuwa wakifika kwenye mabanda ya PSSSF. watapatiwa huduma sawia kama zile zinazotolewa kwenye ofisi za Mfuko zilizoenea nchi nzima Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Kuhusu fursa za Kilimo na Ufugaji, Bi. Rehema, amesema, wamekuja na bidhaa za chai kutoka kiwanda cha Mponde ambacho Mfuko huo umewekeza, lakini pia kwenye eneo la ufugaji, watapata fursa ya kujionea na kununua bidhaa za ngozi zinazozalishwa kwenye kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited ambacho PSSSF inamiliki kwa ubia na Jeshi la Magereza. “Kuna bidhaa kama vile, viatu, mikanda na mabegi hivyo tunawakaribisha sana wanachama na wananchi kupata bidhaa hizo.” Afisa Uhusiano, PSSSF, Bi. Rehema Mkamba.
Pia watakaotembelea banda la PSSSF kwenye viwanja vya Nzuguni Dodoma, wataweza kujinunulia nyama kutoka Machinjio ya kisasa ya Nguru Hills Ranch, yanayomilikiwa na PSSSF kwa ushirikiano na wabia wengine wawili.
Aidha Fursa zingine ni pamoja na kununua nyumba za bei nafuu.