
Rais Samia Suluhu Hassan, amezitaka mamlaka husika kusimamia sheria za ujenzi ipasavyo, akionya kuwa wapo pia wenye mamlaka ambao wanavunja sheria walizotunga.
Ameeleza haya Jijini Dodoma wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Rais Samia ametolea mfano wa eneo la Kariakoo, akieleza jinsi vibali vya ujenzi vinavyotolewa na halmashauri, lakini baadhi ya watu wanakiuka masharti ya vibali hivyo kwa kujenga majumba makubwa zaidi ya ukubwa ulioidhinishwa.
"Kuna majumba yanajengwa ajabu ajabu, mfano mzuri eneo la Kariakoo. Halmashauri kule iwe ya Jiji la Dar es Salaam au halmashauri nyingine wanatoa vibali mtu akishakipata kibali anakwenda kujenga nyumba aliyopewa kibali lakini na rumbesa juu. Rumbesa sasa zimeacha kuwa za mazao ya kilimo zimekwenda kwenye ujenzi, unaona kabisa nyumba imejengwa lakini ina kishubaka kimeongezwa juu"Amesema Rais Samia.