Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kuendelea kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi Wazawa, katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara na madaraja ili kuwajengea uwezo na kufanya uchumi kuwa na mzunguko mzuri ndani ya nchi.
Rais Samia ametoa agizo hilo Kilosa Mjini katika hafla ya ufunguzi wa wa barabara Rudewa - Kilosa (km 24) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Morogoro.
Aidha, Dkt. Samia ameeleza kuwa Morogoro ni mkoa wa kimkakati kwa maendeleo ya miundombinu ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali kupitia TANROADS imeupatia Mkoa huo kiasi cha Shilingi Bilioni 78.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja.
Dkt. Samia ameeleza kuwa umuhimu wa mradi wa barabara ya Rudewa - Kilosa kwa wananchi ikiwemo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na bidhaa na hivyo kuchochea uchumi wa Wananchi wa Kilosa Mjini na kukuza biashara.
Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inakwenda kukamilisha ujenzi wa barabara katika kipande kilichobakia cha kuunganisha Wilaya ya Kilosa na Mikumi katika barabara ya Dumila – Kilosa – Ulaya – Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami katika mradi huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa barabara ya Rudewa - Kilosa (km 24) ni sehemu ya barabara muhimu kwa kuwa inaunganisha Mkoa wa Tanga, Morogoro na Nyanda za Juu Kusini ambapo inaanzia Bandari ya Tanga - Handeni - Mziha - Turiani - Dumila - Kilosa - Mikumi - Ifakara - Mlimba - Lupembe hadi Mkoani Njombe.
Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imetengewa zaidi ya Bilioni 800 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara iliyoathirika kutokana na mvua za El-Nino katika mikoa yote nchini kipindi hiki cha kiangazi ambapo hivi sasa kazi za manunuzi zimeanza kwa ajili ya utekelezaji na Mkoa wa Morogoro ukiwemo.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza barabara ya Dumila – Kilosa – Ulaya - Mikumi (km 142) ni barabara ya Mkoa inayounganisha barabara kuu ya Morogoro – Dodoma katika eneo la Dumila na barabara kuu ya TANZAM katika eneo la Mikumi.
Besta ameeleza ujenzi wa barabara ya Rudewa - Kilosa umetekelezwa na kampuni ya wazawa ya M/s Umoja Kilosa JV yenye muunganiko wa Makandarasi saba (7) Wazawa na Mhandisi Mshauri kampuni ya PIDAEL JV Consulting Engineers ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 45.6 zikihusisha gharama za fidia, ujenzi na usimamizi.