Katika kupambana na maambukizi ya Marburg, Waziri wa Afya nchini Rwanda Dkt. Sabin Nsanzimana amesema nchi hiyo imepokea chanjo 1000 kutoka Kampuni ya Sabin Vaccine kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi hayo, ambapo watu 600 kati ya 700 wamepatiwa chanjo nchini humo.
Waziri Sabin amesema, chanjo hizo zinalenga wafanyakazi wa afya na wale walio katika mazingira hatarishi, hasa wale wanaofanya kazi katika vitengo vya wagonjwa mahututi (ICU) na ambao wanakabiliwa zaidi na hatari ya maambukizi.
Chanjo ya dozi moja ya Kampuni ya Sabin inasambazwa kwa mujibu wa itifaki ya kimatibabu, iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Maadili na Udhibiti ya Rwanda.
Tangu Septemba 27, maambukizi 61 ya virusi vya Marburg yamethibitishwa, watu 14 wamekufa na watu 29 wanaendelea na matibabu.