
Serikali kupitia Wizara ya Fedha, imeombwa kusimamia upatikanaji wa fedha na utoaji wa mikopo ya Halmashauri inayotolewa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wa makundi maalumu, ili kuhakikisha inawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.
Ombi hilo limetolewa wilayani Liwale mkoani Lindi, na Mwenyekiti wa Kikundi cha Tunaweza, Bi. Diana Venant, baada ya kumalizika kwa mafunzo maalum yenye lengo la kuwaongezea mitaji ya biashara na kuwakwamua kiuchumi, yanayotolewa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Vikundi vya Huduma Ndogo za Fedha, Wilaya ya Liwale, Bw. Obadia Anania, aliipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali nchini.
Naye Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Kimaro alisema kuwa Wizara inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha, ili kuhakikisha wananchi wote wanakua na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo kuwa na mazoea ya kujiwekea akiba, kuwa na nidhamu ya matumizi lakini pia kutumia kulingana na bajeti yako.
