Back to top

SERIKALI KUANZA MAHOJIANO RASMI NA WAKIMBIZI

15 October 2024
Share

Serikali ya Tanzania inatarajia kuanza mahojiano ya kina na wakimbizi wa Burundi wanaoishi nchini ifikapo 2025 ambapo mahojiano hayo yatashirikisha wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR). 


Lengo kuu ni kubaini changamoto wanazokabiliana nazo wakimbizi na kutafuta suluhisho la kudumu kulingana na maoni yatakayokusanywa katika mahojiano.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, alipowasilisha ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 75 wa Kamati Tendaji ya UNHCR nchini Uswisi, tarehe 15 Oktoba 2024. 

Mhe. Sillo alibainisha kwamba Tanzania inahifadhi wakimbizi zaidi ya 240,000, wengi wao wakiwa kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alisema serikali imefanikiwa kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi 17,283 kwa mwaka huu, ambapo wakimbizi 12,717 walirudi kwa hiari katika nchi zao za asili, na 4,566 walipatiwa makazi mapya katika mataifa mengine.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake katika kuhifadhi wakimbizi kwa miaka mingi na sasa kujikitika katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa Wakimbizi hao. 

Aidha alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana ili kusaidia wahanga wa migogoro na kuhakikisha wanapata misaada inayohitajika.