Back to top

SERIKALI YAANZA UJENZI WA CHUO CHA MAFUNZO YA MIFUGO SONGWE

26 March 2024
Share

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Wakala wa Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA), imeanza ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mifugo katika mkoa wa Songwe, kitakachogarimu takribani shilingi Bil.1.2 zilizotolewa na Mhe.Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni hatua ya kuongeza idadi ya Maafisa Ugani upande wa sekta ya Mifugo nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo kwa Mkandarasi atakayefanya kazi hiyo Mbozi mkoani Songwe, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ubora wa majengo unaendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali na kumaliza kazi hiyo kwa wakati waliokubaliana.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbozi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe.Farida Mgomi, amewataka wasaidizi wake wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi huyo wakati wote wa ujenzi wa mradi huo huku pia akiahidi kuusimamia kwa karibu  na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya 'Civil Loth Engineering LTD' Mhandisi Robert Lupinda, ambaye ndiye mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ameahidi kukamilisha majengo ya chuo hicho kwa wakati na ubora unaotakiwa huku akiomba ushirikiano wa kutoka kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo.

Kwa Mujibu wa Mhandisi Ujenzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Gabriel Mligo, ujenzi huo unajumuisha jengo la Utawala, bweni na chumba cha mafunzo na utakamilika ndani ya miezi 6 kuanzia hivi sasa.