
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga hadi ifikapo mwaka 2030 iweze kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi chini ya 70 kwa vizazi hai 100,000 kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuongeza vituo vya afya, huduma za dharura za upasuaji na wodi maalum za watoto wachanga.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo kwenye tamasha la kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutunukiwa tuzo ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award iliyofanywa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoani Tanga.
"Shirika la Afya Duniani (WHO) linataka hadi tunapofika mwaka 2030, vifo hivyo viwe vimepungua mpaka kufika 70, sisi kwa muda mfupi tumetoka vifo 556 mpaka kufikia 104, na tunaendelea na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mpaka 2030, tuna uhakika wa kushusha vifo hivyo hadi 70 kwa vizazi hai 100,000," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, tuzo hizo zimekuwa zikitolewa nchini Marekani na ni lazima uende nchini humo ili upewe lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni Rais wa kwanza kupewa tuzo hiyo ndani ya nchi yake kwa heshima kubwa aliyojijengea na kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuokoa vifo vya kina mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweza kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 hadi kufikia vifo 43 kwa vizazi hai elfu 1,000 kwa takwimu za vizazi na vifo vya mwaka 2022.
"Ili kuendelea kupunguza vifo hivyo, tayari Serikali imeshajenga vyumba maalum vya uangalizi wa watoto wachanga wagonjwa (NICU) 362, vituo vya kutolea huduma za afya vimefika elfu 10,044 nchi nzima, vyumba vya upasuaji wa dharula kwa wajawazito 531 ambavyo vimesaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto," amesema Waziri Mhagama.
Vilevile, Waziri Mhagama amesema Serikali imeweza kununua mashine za Ultrasound 970 nchi nzima ambazo zinamuwezesha daktari kujua hali ya maendeleo ya mtoto akiwa tumboni.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa UWT Bi. Zainab Shomari ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujali afya za wananchi wake kwa kujenga vituo vya afya karibu na wananchi ambavyo vimewezesha kufikika ndani ya kilometa Tano (5).
"Mhe. Rais amefanya makubwa ndani ya nchi hii ikiwemo kujenga Hospitali kubwa, vituo vya afya, wodi za wazazi na watoto ambavyo vimewezesha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi," amesema Bi. Shomari