Back to top

SERIKALI YATANGAZA NEEMA KWA WAHANDISI WANAWAKE

21 August 2024
Share

Waziri wa Ujenzi Mhe.Innocent Bashungwa, amesema serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kutoa fursa kwa wahandisi Wanawake, kushiriki kikamilifu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja nchini.

Waziri Bashungwa amezungumza hayo mkoani Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la tisa (9) la wahandisi wanawake, lililoandaliwa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), kupitia Kitengo cha Wanawake na kuwasisitiza Wahandisi Wanawake kuchangamkia fursa hizo.

Bashungwa ameeleza kuwa kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga fedha takribani Bilioni 600 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara, ambapo zinatoa fursa kwa makundi maalum ikiwemo Kundi la Wanawake kutekeleza kazi hizo kwa asilimia 100.

Lakini pia , Bashungwa ametoa wito kwa Taasisi ya Wahandisi Tanzania kupitia Kitengo cha Wahandisi Wanawake kuweka mikakati ya kuhamasisha na kuwahusisha wanafunzi watoto wa kike kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi kujiamini na kujiunga na masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia Julai 2024, Tanzania Bara ina wahandisi 38,233 ambapo kati ya hao wanawake ni 5,006, sawa na 15.07%.

Kwa upande wake  Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zena Said, ametoa wito kwa Wahandisi Wanawake kujiamini, kushirikiana kwa pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali kutoka Sekta mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitengo cha Wanawake kutoka Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Rehana Juma ameeleza kuwa Kitengo hicho kilianzishwa kwa lengo la kuendeleza kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania pamoja na kuhamasisha wanawake kujiunga na fani ya Uhandisi, Sayansi na Hesabu.