Back to top

SERIKALI YATENGENEZA SERA WEZESHI KWA MWANAMKE

01 March 2025
Share

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko , amesema serikali imetengeneza sera wezeshi, sheria na taratibu ambazo zinamwezesha mwanamke kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Dkt. Biteko amesema hayo jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki kongamano maalum kuelekea Maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Wanawake (Pre IWD), ambapo amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wanawake wanaoshiriki katika Sekta ya madini ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume na kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, watu 6,030,575 wanajihusisha na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.

Kufuatia takwimu hizo, wanawake ni 3,094,647 sawa na asilimia 51.3 ya watu wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali katika uchimbaji mdogo wa madini, hususani katika sekta ndogo ya uziduaji, kati ya wachimbaji wadogo milioni moja na nusu, asilimia 27 kati yao ni wachimbaji ni wanawake.

Ametaja jitihada za Rais Samia katika kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo, kuwa ni kutoa kipaumbele wanawake kushiriki katika shughuli zote za Kiuchumi kwa kuwapa  fursa za elimu pamoja na kumiliki rasilimali zilizopo kama vile kupata elimu, fursa za kupata mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kupata vifaa na vitendea kazi na kushiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi.

Amefafanua kuwa ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini ni nyenzo muhimu  katika kukuza mnyororo wa thamani katika jamii na hivyo ni muhimu kutambua na kuthamini mchango wao katika shughuli hizo  na jamii kwa ujumla.

Aidha, taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Sekta ya Madini ikijumuisha na masuala ya gesi, kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 imechangia kwa kiasi kikubwa katika ajira. Ambapo ajira za moja kwa moja 218,353. Kati ya ajira hizo, 176,815 ni wanaume na 41,538 ni wanawake ambayo ni sawa na asilimia 20.

Amesema Serikali imetekeleza na kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo kupitia utekelezaji wa Sera wezeshi, Sheria na taratibu mbalimbali ambapo kupita Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka (2023) na Sheria ya Madini ya mwaka (2017) pamoja na kanuni za ‘Local Content’, Serikali inasisitiza ushirikishaji wa wanawake na kuhakikisha wanapata uwezo rasilimali katika sekta ya madini.

Vilevile, uwezeshaji wa kifedha na kitaaluma, ambapo Serikali kupitia Taasisi zake na wadau mbalimbali ikiwemo  Kamisheni ya Madini Tanzania na Umoja wa Wachimba Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), imesadia kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wanawake mbalimbali ndani na   nje ya nchiambapo mwaka 2023, Serikali iliwapeleka wanawake watano  nchini China kwa ajili ya kujifunza na kutafuta masoko.