
Spika wa Bunge, Dkt.Tulia Akson ameisisitiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) kuhakikisha miradi yote ya barabara inayokamilia inapimwa ubora kwa kutumia vifaa maalum kabla ya Mkandarasi kuikabidhi kwa serikali.
Dkt.Tulia amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akifungua Maonesho ya siku mbili ya sekta ya Ujenzi ambapo amempongeza Rais wa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye uwekezaji wa eneo la miundombinu ya Barabara.


Amesema kuwa mitambo na vifaa vya kisasa iliyonunuliwa hivi karibuni na TANROADS itaisaidia serikali kuondokana na changamoto ya kukabidhiwa MIradi ya Barabara iliyo chini ya kiwango.
Kuhusu Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) amewapongeza kwa kufanya mageuzi ya kuwatafuta wateja waliko na kufanya kazi ya matengenezo kwa saa 24 kwa kutumia Karakana zinazotembea (Mobile Workshop) kuliko ilivyokuwa ambapo walisubiri kupelekewa kazi za kufanya kwenye maeneo yao.
