
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Tanzania imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa mlipuko wa Marburg na ameutangazia Umma wa Watanzania kuwa ugonjwa huo umeisha kutokana na kutokuwepo kwa mgonjwa mwengine yeyote tangu mgonjwa wa mwisho alipopatikana tarehe 28 Januari, 2025 na hadi kufikia tarehe 11 Machi, 2025 siku 42 zimepita.
Waziri Mhagama amethibitisha hayo leO alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wilayani Biharamulo, Kagera kwamba siku 42 zimepita tangu mgonjwa wa mwisho alipofariki mgonjwa wa mwisho afariki na kisayansi Tanzania inakidhi vigezo vya kutangaza kuwa mlipuko huo umeisha.
"Tarehe 20 Januari, 2025, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliutangazia umma na jamii ya Kimataifa juu ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliotokea katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, naomba nichukue fursa hii leo tarehe 13 Machi, 2025 kuutangazia umma na jamii ya Kimataifa kuwa, sasa Tanzania haina mlipuko wa ugonjwa wa Marburg," amesema Waziri Mhagama.
"Ugonjwa wa “Marburg” ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayotokana na virusi ambavyo husababisha kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na husambaa kwa haraka kwa kupitia kugusa majimaji ya mwili wa mtu au mnyama aliyeathirika na ugonjwa huo ambao husababisha madhara mbalimbali ikiwemo ulemavu na vifo," amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama ameendelea kuwakumbusha Watanzania juu ya kuchukua tahadhari kwakuwa nchi zinazotuzunguka zinaendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Mpox na Ebola, hivyo nchi yetu pia ipo kwenye hatari kutokana na mwingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na uwepo wa mipaka ya moja kwa moja baina ya nchi hizi.
"Hivyo naomba niwasihi wananchi wote kuendelea kushirikiana na wataalam wa afya na mamlaka husika ili kuendelea kutekeleza afua za kujikinga na magonjwa haya, na sisi kama Serikali tumedhamiria kuhakikisha tunaimarisha zaidi huduma za tiba kwa wagonjwa wakati wa dharura na mlipuko," amesema Waziri Mhagama.
Pia, Waziri Mhagama amesema dhamira ya Serikali ya kujenga hospitali maalum kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa ya mlipuko katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera iko palepale pamoja na kuongeza maabara jongezi yenye uwezo wa kupima magonjwa ambukizi ya mlipuko ili kujihakikishia kinga na udhibiti zaidi wa magonjwa hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajat Fatma Mwassa ametoa shukran kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akielekeza na kutoa ushauri wa jinsi ya kudhibiti ugonjwa wa Marbug pamoja na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama aliyekuwa msimamizi wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais na hatimaye kuumaliza ugonjwa huu.
"Lakini pia Mhe. Waziri tunakushukuru kwa kuweka kipaumbele cha kujenga hospitali ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko hapa Biharamulo, kuwa na wodi ya kwanza ya kuwatenga wagonjwa wa mlipuko ambayo itaanza kujengwa hapa pamoja na kutupatia vifaa vya mobile lab kwa ajili ya kupima magonjwa mbalimbali ya vihatarishi na sisi kama mkoa tutaendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa magonjwa haya hujirudia," amesema Hajat Mwassa.
Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kuwa Serikali imeimarisha miundombinu mbalimbali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo uimarishaji wa maabara zenye uwezo wa kupima magonjwa ya mlipuko hasa za Taifa, utolewaji wa elimu ya afya kwa umma hasa katika mikoa inayopakana na nchi jirani pamoja na upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.
"Mhe. Waziri, katika jitihada hizi tumeshirikiana na wenzetu wa Wizara za kisekta pamoja na wadau wakiwemo wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari pamoja na wadau wa maendeleo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Charles Sagoe-Moses.