#MICHEZO: Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Prof. Palamagamba John Kabudi, amesema Tanzania ipo tayari kwa ajili ya uwenyeji wa mashindano ya CHAN yanayotarajiwa kuanza tarehe 1 hadi 28 Februari 2025 kwa kuwa maandalizi yake yamefikia 99% hadi sasa.
Prof. Kabudi ameyasema hayo alipokagua miundombinu ya viwanja hivyo vya Gymkana, Major general Isamuyo, na uwanja wa Law school ambapo amesema kuwa, asilimia kubwa ya ujenzi huo umekamilika na kuagiza machache yaliyobaki kutimizwa kwa wakati.
Waziri Kabudi amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa viwanja vya Mazoezi ya michuano ya CHAN vilivyopo jijini Dar es Salaam huku akiwataka SUMA JKT kuhakikisha kazi hiyo inamalizika kwa wakati.
Aidha, Waziri Kabudi amewasifu SUMA JKT kwa kutumia weledi wao kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa muda sambamba na kukidhi mahitaji ya shirikisho la mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Akiongea kuhusu umuhimu wa mashindano hayo, Waziri Kabudi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027 kwani mashindano haya yataipa heshima nchi yetu kimataifa na Sekta ya Michezo kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajab Mabele ameishukuru Serikali kwa kuliamini Jeshi letu na kuipa kazi hiyo kwa mara ya kwanza, huku akiahidi kufanya kazi zilizosalia kwa masaa 24 na kukamilisha ujenzi wote mnamo Januari 21, 2025.
Kadhalika, Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania Bw. Wallace Karia akiongelea adhma ya ziara hiyo ni hakikisha maandalizi yamekamilika na amepongeza juhudi za Serikali katika kuinua michezo nchini huku akiomba kazi hiyo iliyosalia ikamilishwe kwa wakati ili kutimiza dhamira ya kuwa wenyeji wa CHAN 2025.
Mashindano haya ya CHAN yanatarajiwa kuanza Februari Mosi, 2025 huku Nchi ya Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja watashirikiana kuwa wenyeji wa michuano hiyo ya kimataifa ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki kama wenyeji.