Back to top

TANZANIA KUFUTA HISTORIA YA VIJIJI KUTOKUWA NA UMEME

16 August 2024
Share

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewahakikishia Watanzania kuwa, Serikali itaendelea kupeleka huduma ya umeme katika maeneo yote nchini ili watanzania waweze kuboresha shughuli za kiuchumi ambapo amesema upelekaji wa umeme kwenye Vijiji ukikamilika, nguvu kubwa itaelekezwa kwenye usambazaji wa umeme kwenye Vitongoji. 

Mhe. Kapinga ameyasema hayo wakati akizindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Mpingi Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

"Ni dhamira ya Mhe. Rais kuhakikisha Vijiji vyote 12,318 nchini vinapata umeme, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), tumebakisha chini ya Vijiji 151 kuvipelekea umeme na kazi inaendelea." Amesema Mhe. Kapinga

Mhe. Kapinga ameongeza kuwa Serikali inakwenda kufuta historia ya Vijiji vya Tanzania kutokuwa na umeme kutokana na Vijiji vyote kwenda kufikiwa na nishati hiyo.

Awali,  Mha.Robert Dulle ambaye ni Msimamizi wa miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Ruvuma alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa umeme kwa kuunganisha kwa gharama ya shilingi 27,000 tu. 

Aidha, amewaasa wananchi kutunza miundombinu ya umeme hasa kipindi cha utayarishaji wa mashamba ambapo miundombinu mingi huathirika kwa kuchomwa moto.