
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake inatekeleza mfumo wa miundombinu ya Kitaifa ya taarifa za kijiografia ambao kukamilika kwake kutaifanikisha nchi kuwa na ramani mpya ya Tanzania itakayoendana na mabadiliko mbalimbali ya kidunia.
Akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la mwaka 2023, Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Rais Samia amesema kuichora ramani mpya ya Tanzania kutawezesha kupanga mipango ya nchi kidigitali na kuondoa migongano ya kisekta katika mipango na matumizi ya rasilimali mbalimbali.
Akizungumzia utekelezaji wa mipango mingine mbalimbali ya sekta ya ardhi, Rais Samia amesema awamu yake kwa kutambua changamoto za ardhi iliongeza bajeti ya Wizara ya ardhi kutoka Bilioni 133.6 mwaka 2020/21 hadi kufikia Bilioni 171.4 mwaka 2024/25, suala ambalo limewezesha kuimarika kwa usalama wa milki za ardhi, upimaji wa viwanja, mashamba makubwa pamoja na kupima mipaka ya vijiji sambamba na kufanyika mwa sensa ya majengo kwa mara ya kwanza tangu kupatikana kwa uhuru miaka zaidi ya sitini iliyopita.