Back to top

TANZANIA YAUNGA MKONO AJENDA ZA UN TOURISM

23 July 2024
Share

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeunga mkono ajenda za Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kuhusu uwekezaji wa kimkakati katika rasilimali watu, kwenye elimu na ujuzi pamoja na ajenda ya usalama wa maeneo ya utalii, lengo likiwa ni kuibadilisha Afrika kwa siku zijazo kupitia ujuzi wa elimu na uwekezaji wa kimkakati.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Angellah Kairuki, alipokuwa akichangia mjadala wa ajenda hizo kwenye mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Utalii wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika (67 CAF) unaoendelea kwenye hoteli ya Radisson Blue Jijini Livingstone Zambia.

Amesema kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii nchini Tanzania, ambacho kipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kimewekeza katika kuwajengea uwezo wakufunzi na kushirikiana na taasisi nyingine za kimataifa, katika utoaji wa mafunzo kwa kubadilishana uzoefu lakini pia kuboresha matumizi ya teknolojia ili kufikia malengo.

Kuhusu Usalama wa maeneo ya utalii, Mhe. Kairuki ameweka bayana kuwa Tanzania inatumia Jeshi la Polisi na imeanzisha vitengo maalum vya kidiplomasia vinavyoshughulikia masuala ya usalama katika sekta ya utalii .

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Usafirishaji Watalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo amesema lengo la kushiriki mkutano huo ni kutafuta fursa za kupata wawekezaji kwa ajili ya Sekta ya Utalii nchini Tanzania.  

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, wataalamu katika Sekta ya Utalii, wawakilishi wa taasisi za fedha na huduma za kifedha na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi wanaosimamia na kuendeleza mabadiliko chanya katika Sekta ya Utalii Barani Afrika.