Back to top

TUZO YA RAIS SAMIA YATANGAZWA MALAWI

10 February 2025
Share

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, akiwa katika Mkutano wa 74 wa Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC) ameitangaza Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupunguza  vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80. 

Wakati akitangaza tuzo hiyo Waziri Mhagama amesema utafiti wa Demografia na Afya Tanzania wa mwaka 2022 unaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 80 kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 hadi vifo 104 mwaka 2022. 

Amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepewa Tuzo hiyo ya 'GOALKEEPERS by Gates foundation' kutokana na uongozi wake mahiri katika kupunguza vifo vya mama,  mtoto mchanga na mtoto, ambapo ameendelea kuboresha na kuweka kipaumbele katika huduma za Afya ya kundi hilo. 

"Maendeleo ya Tanzania katika kupunguza vifo vya uzazi na watoto ni uthibitisho wa nguvu ya kujitolea pamoja na ushirikiano kwa kuhakikisha kuwa hakuna mwanamke au mtoto anayefariki kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, tuendelee kufanya kazi pamoja kama kanda ili kufikia malengo yetu ya pamoja ya afya na kulinda ustawi wa watu wetu wote," amesema Waziri Mhagama. 

Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali ya Tanzania inazingatia kikamilifu na imejitolea kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ya mwaka 2030, hususan malengo ya kupunguza vifo vya uzazi hadi chini ya 70 kati ya watoto 100,000 wanaojifungua, vifo vya watoto chini ya umri wa miaka Mitano hadi chini ya 25 kwa kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wachanga hadi watoto 10.

"Malengo haya yameunganishwa kikamilifu katika sera zetu za kitaifa ikiwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2020-2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021-2025), Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya V (HSSP V, 2021-2026) pamoja na Mpango wa Taifa wa RMNCAH (Mpango Mmoja III, 2021-2026i).