Back to top

UCHUMI WA BULUU NA MKAKATI KUIMARISHA SEKTA UVUVI

29 August 2024
Share

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwaongoza Mawaziri zaidi ya 70 kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), kujadili masuala mbalimbali ya uchumi wa buluu na kuweka mkakati wa pamoja kuimarisha sekta ya uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amebainisha hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa Uvuvi, Bahari na Maji ya Ndani kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki utakaofanyika Jijini Dar es Salaam Septemba 9-13, 2024.

Waziri Ulega amesema mkutano huo utafunguliwa na Mhe. Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan Septemba 11 na umepangwa kufanyika sambamba na Kongamano la Kimataifa kuhusu Mikakati ya Uboreshaji wa Mnyororo wa Uzalishaji wa Vyakula vya Majini ulioandaliwa na Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (FAO).

Ameongeza kuwa mkutano huo pia utajumuisha Wataalam wa sekta ya uvuvi kutoka nchi wanachama na ulimwenguni kwa ujumla wake, Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali, Taasisi za Kikanda, Watafiti, Vyuo Vikuu, na Wavuvi Wadogo ambao ndiyo wahusika wakuu wa mkutano huo.
 
Kwa Mujibu wa Waziri Ulega mkutano huo utaleta nchini manufaa mengi ikiwemo Kufungua fursa za uwekezaji kwenye uchumi wa buluu hususan kwenye maeneo makuu mawili ya uvuvi na ufugaji samaki, kuendelea kuboresha mahusiano ya matumizi ya rasilimali za maji ya asili na zile za ukuzaji viumbe maji, baina ya wadau wetu wale wa mataifa wanachama.