Back to top

UJENZI DARAJA LA MKILI NA MITOMONI KUANZA RUVUMA

27 September 2024
Share

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS),imesema ipo katika hatua ya kumtafuta Mkandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa madaraja mawili, ambayo ni Daraja la Mkili lenye urefu wa mita 20, pamoja na Daraja la Mitomoni lenye urefu wa mita 80, ambalo litaunganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Vijijini.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameyasema hayo  wakati akizungumza na wananchi Wilayani Nyasa mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dk. Samia Suluhu Hassan kufungua barabara ya Mbinga – Mbamba Bay (km 66).

Ujenzi wa madaraja hayo unajiri, kufuatia ziara aliyoifanya Waziri Bashungwa mkoani Ruvuma Januari 26, 2024, ya kukagua miundombinu ya barabara kutokea Songea Mjini hadi kufikia Wilaya ya Nyasa kupitia barabara ya Likuyufusi - Mtomoni (km 124) inayoenda kujengwa sehemu ya kwanza Likuyufusi - Mkayukayu (km 60) kwa kiwango cha lami pamoja na kukagua madaraja ya Mkenda na Mitomoni.

Baada ya kukagua maeneo hayo, Waziri Bashungwa alitoa miezi miwili kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa daraja la zege katika eneo la Mitomoni ili wananchi wa maeneo hayo waondokane na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.