Back to top

UKAGUZI WA VYAKULA VYA MIFUGO NI ZOEZI ENDELEVU

30 September 2024
Share

Meneja wa Maabara Kuu ya Veterinari, kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Geofrey Omarch, amefanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula hivuo katika Wilaya ya Kinondoni, mkoani wa Dar Es Salaam, kwa lengo la kufuatilia ubora wa vyakula vya Mifugo vinavyosindikwa pamoja na kujiridhisha taratibu za usindikwajwi wa vyakula hivyo.

Dkt. Omarch aliongeza kuwa TVLA kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inalenga kuwalinda watumiaji wa vyakula hivyo ili kulinda ubora wa vyakula vinavyozalishwa vitokanavyo na zao la Mifugo pamoja na kuongeza soko la Mifugo kimataifa.

“Tumekuwa tukifanya ukaguzi huu mara kwa mara kwa wasindikaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya Mifugo ili watumiaji wa mazao hayo wawe salama wakati wote. TVLA imedhamilia kuwapitia wazalishaji wote Tanzania nzima kwa nyakati tofauti ili kujiridhisha kile kinachozalishwa kama kinakidhi ubora, kukagua marighafi za uzalishaji, hatua za uzalishaji pamoja na kukagua vibali vya uzalishaji.” Alisema Dkt. Omarch.

Baadhi ya wazalishaji wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kinondoni wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara kwani ukaguzi huo unaowaongezea umakini kwenye uzalishaji wa vyakula.

Sambamaba na hilo wameiomba Serikali kutochoka kwenda kuwakagua na kuwapa ushauri na kuendelea kuwadhibiti baadhi ya wazalishaji ambao sio waaminifu wanaowaharibia soko la vyakula kwa kuzalisha vyakula vyenye mapungufu na kuvipiga chapa za kampuni zingine.

Wakala ya Maabara ya Veterinali Tanzania (TVLA) imekuwa ikifanya ukaguzi wa vyakula vya mifugo mara kwa mara kwa wazalishaji, wauzaji na pamoja na wanunuzi wa vyakula vya Mifugo kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi za Wakuu wa Mikoa pamoja na Halmashauri.