Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, kwa uamuzi wao wa kutenga vitalu 279 kwa ajili ya kuwapangisha wafugaji, ili waweze kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija.
Waziri Ulega ametoa pongezi hizo, wakati wa kikao chake na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, kilichofanyika wilayani humo.
Ameeleza kuwa ni muhimu wafugaji kuwa na maeneo yao ya kufugia, ikiwa ni pamoja na kulima malisho ya mifugo yao kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuepuka migogoro ya mara kwa mara, baina yao na wakulima.
Katika hatua nyingine, wakati wa kikao baina yake na wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, cha kusikiliza kero na changamoto zao, alikemea vitendo vya kibabe vinavyofanywa na baadhi ya wafugaji wilayani humo ikiwemo kuwapiga bakora wakulima.
Waziri Ulega yupo ziarani mkoani Ruvuma, akikagua shughuli mbalimbali za maendeleo, zinazoendelea kufanywa mkoani humo, hususani kwenye sekta ya mifugo na uvuvi.